Askari Mgambo, Jumanne Athuman ametiwa mbaroni na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa katavi manispaa ya Mpanda kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya elfu thelathini za kitanzania.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU, Faustine Maijo ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi katika eneo la Yerusalemu kata ya Kazima, manispaa ya Mpanda.
Amesema mtuhumiwa Athuman ambaye ni askari mgambo mwenye namba MG 426588 katika manispaa hiyo alikamatwa baada ya TAKUKURU kupewa taarifa kutoka kwa mlalamikaji.
“Mgambo huyo alitaka apatiwe sh. 30,000 ikiwa ni kishawishi cha kumfungulia duka lake mlalamikiwa baada ya mtuumiwa kulifunga kwa madai kuwa hakuwa na leseni ya biashara” ameeleza Maijo.
Na kuongeza kuwa ” Hivyo aliomba fedha hizo kama rushwa ili mlalamikaji aendelee kufanya biashara yake bila leseni kwenye duka lake ambalo lipo kwenye mtaa wa Yerusalemu”
Amesema kufuatia kupata taarifa hizo waliandaa mtego ambao uliweza kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akipokea rushwa ya elfu thelarhini kutoka kwa mlalamikaji.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Katavi kujibu tuhuma zake.
Aidha TAKUKURU mkoa wa Katavi imetoa wito kwa watumishi wa umma na jamii kujishughulisha na kazi halali za kuwaingizia kipato na kuacha vitendo vya rushwa.