Rais wa Kenya, William Ruto, amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga mara atakaporejea nchini humo toka Tanzania kushiriki mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu rasilimali watu.
Rais Ruto ameyasema hayo kupitia ujumbe wake aliouchapisha kwenya ukurasa wake wa Twitter, ambapo kwamba, “kama unavyojua siku zote, nipo tayari kukatana nawe ana kwa ana wakati wowote utakaokufaa.”
Hatua hiyo, inakuja baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya kuipinga Serikali ambayo yamezua taharuki Kitaifa na Kimataifa, ambapo takriban watu 50 waliuawa wakati wa vurugu tangu mwezi Machi 2023, lakini takwimu rasmi zinasema ni watu 20 ndio waliouawa.
Muungano wa Azimio la Umoja, umefanya maandamano kwa jumla ya siku tisa dhidi ya Serikali ambayo yamekuwa yakibadilika mara kwa mara kuwa uporaji na mapambano kati ya Polisi na Waandamanaji.
Hata hivyo, Odinga aliomba maandamano yasitishwe mwezi Aprili na Mei baada ya Ruto kukubali kufanya mazungumzo lakini yalikwama huku muungano wa Azimio ukiandaa duru kadhaa za maandamano mwezi huu.