Baada ya kuanza vizuri Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuichapa Ihefu FC bao 1-0, Kocha Msaidizi wa Ruvu Shooting Rajab Nakuchema ameitumia salamu Mtibwa Sugar, kuelekea Mzunguuko wa pili kesho Ijumaa (Agosti 19).

Ruvu Shooting walianzia ugenini Uwanja wa Highland Mkoani Mbeya na kuwashangaza wengi kwa matokeo waliyoyapata, hali ambayo iliongeza morari kwa Wachezaji na Benchi la Ufundi la klabu hiyo.
Ruvu Shooting itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar Jumapili (Agosti 21)Uwanja wa Manungu Complex Mkoani Morogoro.

Kocha Nakuchema amesema baada ya kupata ushindi dhidi ya Ihefu FC wameendelea kujiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, huku wakiwa na matarajio makubwa ya kuendelea kufanya vizuri katika viwanja vya ugenini.

“Maandalizi yetu yapo vizuri kwa ajili ya kukabiliana na mchezo wetu dhidi ya Mtibwa, tumejipanga kupambana kama ilivyokua dhidi ya Ihefu FC, lengo letu ni kupata alama sita kabla ya kurejea katika Uwanja wetu wa nyumbani.”

“Wachezaji wetu kwa ujumla wana hali nzuri wakiwa na morari kubwa kutokana na kuanza vizuri ligi kwa kupata ushindi ugenini dhidi ya Ihefu FC, tuna majeruhi mmoja ambaye ni Sadat Mohamed, huyu pia aliukosa mchezo uliopita.”

“Tunawaheshimu wapinzani wetu, kikubwa tunataka alama tatu, hivyo tutahakikisha tutaingia mchezoni kwa tahadhari kubwa.” amesema Kocha Nakuchema

Siku ya sensa ni mapumziko: Rais Samia
Ujumbe wa Marekani watua Kenya kurekebisha mambo