Mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Ihefu FC dhidi ya Naumungo FC utachezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Mchezo huo awali ulipangwa kuchezwa Uwanja wa Highland Estate mkoani Mbeya, lakini hatua ya kufungiwa kwa Uwanja huo na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ kwa kukosa vigezo vya kikanuni, kumeufanya mchezo huo kuuhamishia Uwanja wa Uhuru.

Kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Ihefu FC Zuberi Katwila amesema tayari ameshaanza maandalizi ya kikosi chake na wachezaji wote wapo vizuri kuikabili Namungo FC.

“Mpaka sasa tumejiandaa vizuri na tupo tayari kuelekea mchezo ujao, hatuna majeruhi, wachezaji wote wapo sawa.”

“Kutokana na kuwa tulichelewa kuchagua Uwanja, TFF wenyewe wametuchagulia kucheza Dar es salaam, kwetu ni sawa tu, hatuangalii tutacheza wapi zaidi ya kusaka ushindi.” amesema Kocha Katwila.

Ihefu FC ilianza vibaya Mshike Mshike wa Ligi Kuu msimu huu kwa kupoteza nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting kwa kufungwa 1-0, huku Namungo FC ikianza kwa sare ya 2-2 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mtunisia: Kwa simba hii muda utaongea
Kenya: Wakenya wasubiri suluhu mzozo wa matokeo