Baada ya tume ya uchaguzi nchini Kenya kumtangaza William Ruto kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha urais, Wakenya sasa wanasubiri suluhu ya mzozo wa uchaguzi baada ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga kuyakataa matokeo hayo.

Akihutubia wanachama wa muungano wake jijini Nairobi, William Ruto amewapongeza wafuasi wake kwa kumpa mamlaka kwa kusema, hana sababu ya kuitenga jamii yeyote ya Wakenya na kwamba watashirikiana kulijenga Taifa hilo.

“Mwaka 2017, tulikuwa na 25% katika kaunti 34, mwaka huu, tumeshinda 25% katika kaunti 39; mamlaka haya mapana yanakuja kwangu na wajibu mkubwa kwa kila Mkenya kutambua kwamba hakutakuwa na nafasi ya kumtenga mtu yoyote ya Jamhuri ya Kenya.”

Ruto amezungumza na wanahabari baada ya kukutana na wanachama wa muungano wake wa kisiasa na kusema, “utawala wangu hautahusiana na uhuni tuliouona, vitisho ambavyo tumeona, hofu iliyopandwa kote nchini licha ya kuwepo na mitazamo tofauti ya kisiasa lakini tunarudisha nchi yetu ya kidemokrasia.”

Ruto, naibu rais wa Kenya, alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Kenya, lakini tume ya uchaguzi iligawanyika hadharani dakika chache kabla ya tangazo hilo kwa Makamishna wanne kati ya saba walioteuliwa mwaka jana na Rais Uhuru Kenyatta.

Makamishna hao wa IEBC, walisisitiza kuwa mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chabukati aliwatenga katika hatua za mwisho kabla ya tangazo lake huku mwanasiasa mkongwe Raila Odinga akiyaita matokeo hayo kuwa ni batili na kuahidi kuyapinga.

Makamishna wa IEBC waliodai kutengwa na Mwenyekiti wa tume hiyo wakati wa zoezi la utoaji matokeo ya Urais. Picha na The Standard.

Mgombea mwenza wa Odinga, Martha Karua aliwaambia waandishi wa Habari kuwa “Ushindi wetu umeahirishwa, lakini unakuja nyumbani,” “ambapo sasa umoja huo wa Azimio una siku saba za kuwasilisha katika Mahakama ya Juu pingamizi hilo, huku IEBC ikiwa na siku 14 za kutoa uamuzi juu yake baada ya kuyapokea.

Ihefu FC Vs Namungo FC kupigwa Uhuru Dar
Waziri Mkuu atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 3