Kikosi cha Ruvu Shooting Rasmi kitaanza kutumia Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro kama Uwanja wake wa nyumbani, baada ya Benchi la Ufundi kuridhia maamuzi ya Uongozi wa Klabu hiyo.
Awali Ruvu Shooting ilikua ikiutumia Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kama Uwanja wake wa nyumbani, Kufuatia Uwanja wake rasmi wa Mabatini uliopo Mlandizi kufungiwa na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ kwa kushindwa kukidhi vigezo.
Kocha Mkuu wa Maafande hao kutoka Mlandizi Mkoani Pwani Mbwana Makata amesema, wana imani na Uwanja wa Jamhuri, na wataanza kuutumia kwenye mchezo ujao dhidi ya KMC FC utakaopigwa Jumapili (Februari 05).
“Tuko kwenye Uwanja mpya ambao ni wa Morogoro, ni Uwanja ambao utakuwa wa nyumbani kwetu kwa michezo minne iliyobaki na mmoja wapo ni huo dhidi ya KMC,”
“Tutahakikisha tunapambana kwa hali na mali nafasi tunazopita tuweze kuzitumia na kupunguza makosa ambayo yataweza kuwapa nafasi wapinzani wetu.”
“Tunaona ni sehemu ya utulivu kwa wachezaji wetu kuweza kukaa kwa pamoja, pia tutaweza kuutumia Uwanja huu kwa matumizi mazuri zaidi kwa sababu unakuwa ni uwanja wakwetu, tofauti na Uhuru ambao unatumiwa na timu zaidi ya timu tatu, kwa hiyo itatusaidia kufanikisha lengo la kupambana na kupata alama zitakazotusaidia.” amesema Kocha Makata
Hadi sasa Ruvu Shooting iliyocheza michezo 21, inaburuza mkia wa msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 14, ikishinda michezo mitatu, ikitoka sare mitano na kupoteza kumi na tatu.