Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kitakachoivaa Singida Big Stars keshokutwa Ijumaa (Februari 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Phiri alipata jeraha ya mguu wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Suga mwishoni mwa mwaka 2022, hali ambayo ilipelekea kukosa michezo kadhaa, kabla ya kuanza mazoezi mepesi.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema: “Wachezaji wetu waliokuwa majeruhi wamerejea wakiwa tayari kasoro Moses Phiri ambaye amerudi mazoezini, lakini hajaanza mazoezi na wenzake.”

“Enock Inonga, Jimmy Baleke na Peter Banda wamerudi kikosini na wamefanya mazoezi na wenzao kwa asilimia 100. Kiufupi hali ni shwari.”

“Tunakwenda katika mechi mechi ya Ijumaa dhidi ya Singida Big Stars tukiwa sawasawa. Tunahitaji kushinda mchezo huu ili kutengeneza morali kuelekea mechi za Kimataifa tunazokwenda kuzianza mwezi huu “

Baada ya mchezo dhidi ya Singida Big Stars, Simba SC itacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Al Hilal ‘Omdurman’ ya Sudan, Jumapili (Februari 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC itacheza mchezo huo, ikijiandaa na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi, ambapo itachea dhidi ya Horoya AC Februari 11 mjini Conakry-Guinea, katika Uwanja wa General Lansana Conté.

Al Hilal ‘Omdurman’ nao watakuwa wanajiandaa na mchezo wa Kundi B dhidi ya Mabingwa wa Afrika Kusini Mamelodi Sundowns utakaopigwa mjini Pretoria katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Februari 11.

SportPesa: Young Africans imekiuka makubaliano
Mashambulio mawili ya waasi yauwa raia 28