Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Rwanda amewaachia huru watu 1,673 waliokuwa wanashikiliwa katika magereza mbalimbali nchini humo, ikiwa ni hatua ya kupunguza msongamano ili kupambana na maambukizi ya virusi vipya vya corona (covid-19).
Idadi hiyo ya wafungwa iliyoachiwa jana, Aprili 27, 2020 ni kubwa zaidi tangu Serikali ya nchi hiyo ilipotangaza mpango wa kuwaachia huru baadhi ya watu wanaoshikiliwa.
Zoezi hilo limefanywa na Mamlaka ya Mashtaka ya Taifa (NPPA) kwa kushirikiana na Mahakama, Jeshi la Polisi na Shirika la Upelelezi.
Mwendesha Mashtaka Mkuu, Aimable Havugiyaremye alisema kuwa wenye sifa za kuachiwa ni wale ambao makosa yao yanaruhusu kulipa faini bila hata kufikishwa mahakamani; na kundi la pili ni watu wanaoshikiliwa ambao wanaweza kuachiwa kwa masharti yanayokubalika kisheria.
Hata hivyo, wanaoshikiliwa kwa makosa makubwa ya jinai hawatafaidika na maelekezo hayo ya Mwendesha Mashtaka Mkuu.
“Ingawa tumefungiwa ndani, watu wengine bado wanaendelea kufanya makosa na wanapelekwa kwenye vituo vya kuwashikilia. Kama hatua za awali, kwa kuzingatia mpango wa kupunguza watu magerezani, inawezekana kabisa kuendelea kuwapunguza wengine kama wanaokamatwa wataendelea kuongezeka,” Msemaji wa NPPA, Faustin Nkusi aliiambia The New Times.
Alisema kuwa wanaoachiwa wanapewa masharti ikiwa ni pamoja na maelekezo ya wapi wasipopaswa kwenda na jinsi ya kuishi kwa kujitenga kwa muda.