Serikali ya Rwanda imetoa hati ya kimataifa ya kumkamata aliyekuwa mpelelezi wa nchi hiyo, Aloys Ntiwiragabo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Mwendesha Mashtaka wa Rwanda, Aimable Havugiyaremye amewaambia waandishi wa habari kuwa vyombo vya usalama vinaendelea kupeleleza mashtaka dhidi yake na vimekuwa vikishirikiana na kitengo cha usalama cha Ufaransa kinachoshughulikia makosa ya jinai.
Ufaransa iliamua kuongeza nguvu za kumsaka mtuhumiwa huyo, baada ya chombo cha habari cha nchini humo kiitwacho ‘Mediapart’ kuweka mtandaoni kipande cha video kinachomuonesha akiwa anatembea kwenye mitaa ya jiji la Orleans, Kilometa 100 kutoka jiji la Paris.
Kabla Mediapart hawajaweka video hiyo mitandaoni, Ufaransa na Rwanda hawakuwa wanamtafuta kwa nguvu mtuhumiwa huyo ambaye alitajwa na Mahakama ya kimataifa ya mauaji ya kimbari ya Rwanda (ICTR).
Katika miaka kadhaa iliyopita, nchi hizo ziliamua kuahirisha hati za kumkamata Havugiyaremye.
Takribani watu 800,000 wengi wao wakiwa ni Watutsi waliouawa wakati wa mauaji ya kimbari.