Mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Gwambina FC Mwinyi Zahera, amesema beki wa kati wa Tanzania Kelvin Yondani bado ana uwezo mkubwa wa kucheza soka, tofauti na anavyozungumzwa katika vijiwe vya soka la Bongo.

Zahera ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Young Africans, na baadae kutimuliwa kufuatia kushindwa kufikia malengo ya kufanya vyema kwenye michuano ya kimataifa, amesema beki huyo bado ana uwezo wa kucheza soka la ushindani kwa misimu mingine miwili.

“Mnasema Kelvin amezeeka, mnapaswa kuangalia nani anacheza naye kwenye nafasi ya beki, nani ana akili na mpira, na nani ana uwezo wa kucheza michezo ya kimataifa,”

Kelvin bado ana uwezo sana kisoka ninashanga watu wanavyombeza kwa kusema amezeeka, kwa hapa Tanzania huyu anaendelea kuwa beki ambaye ninamuamini, ana anafasi ya kucheza kwa ufanisi mkubwa kwa zaidi ya msimu mmoja.” Amesema Zahera

Katika hatua nyingine Kocha Zahera amesema mshambuliaji kutoka DR Congo David Molinga (Falcao), alipaswa kupewa nafasi na uongozi wa Young Africans kwa msimu mmoja zaidi, ili kuendelea kudhihirisha uwezo wake wa soka.

“Niliwaambia waandishi wa habari, Molinga atafunga zaidi ya mabao 15 na amefanya hivyo, sasa leo unamuondoa kwenye kikosi kama cha Yanga, wakati yeye ndio kinara wa kufunga mabao?” Alihoji kocha huyo

“Walipaswa kumpa nafasi nyingine ya kucheza ili kuonyesha uwezo wake kisoka, naamini Molinga alikua na kila sababu ya kuendelea kuwafurahisha mashabiki wa Yanga.”

“Amecheza michezo michache sana kwa msimu uliopita, na kulikua hakuna sababu ya kumkalisha nje, hakuna sababu kabisa. Wakati mwingine nilimuuliza kwa nini huchezi, aliniambia hana tatizo lolote lakini imekua kawaida kuwekwa benchi.” Amesema Zahera.

Kelvin Yondani na David Molinga ni sehemu ya wachezaji walioachwa na Young Africans katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Wachezaji wengine walioachwa Young Africans katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni pamoja na Mrisho Ngasa, Jaffary Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vicent, Papy Tshishimbi na Mohamed Issa.

Wengine ni Ally Mtoni, Muharami Issa, Yikpe, Ali Ali, Patrick Sibomana, Eric Kabamba, Juma Abdul na Raphael Daud.

Mwinyi ataja sababu za kugombea urais Zanzibar
Fraga: Puuzieni mitandao ya kijamii, bado nipo Simba SC