Kikosi cha KMC FC leo Jumatatu (Januari 09) kimeanza Mazoezi kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, siku ya Ijumaa (Januari 13) katika Uwanja wa Manungu Mkoani Morogoro.
Rasmi Kikosi cha KMC FC kilianza kukusanyika jana Jumapili (Januari 08) jijini Dar es salaam, baada ya mapumziko ya sikukuu za mwisho wa mwaka 2022 na mwanzo wa mwaka 2023.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa KMC FC Christina Mwagala amesema mbali na Wachezaji kukusanyika tangu jana, Kocha Mkuu Thierry Hitimana naye amerejea jijini humo akitokea nchini Rwanda ambako alifiwa Mdogo wake.
Hata hivyo Mwagala amesema, Maandalizi ya KMC FC kuelekea mchezo dhidiya Mtibwa Sugar yanawakosa wachezaji saba kutokana na sababu mbalimbali ambao ni Sadalah Lipangile, Ibrahimu Ame, Matheo Anton, Steve Nzingamasabo pamoja na Ismail Gambo ambapo wote ni kutokana na changamoto za kifamilia huku Emmanuel Mvuyekure na Hance Masoud wakiendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha ya muda mrefu.
“Tumeanza mazoezi leo baada ya mapumziko mafupi ambayo tuliwapa wachezaji katika kipindi hiki ambacho Timu zipo kwenye mapumziko kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, kikubwa tunakwenda kwenye mchezo mgumu ambao tutakuwa ugenini na ndio mana tumekuwa na muda mfupi wakupumzika lengo likiwa kujiandae vizuri kwa ajili ya kupata matokeo chanya.”
“Tutakuwa na mchezo mgumu ambapo ukizingatia tutakwenda tena ugenini baada ya kutoka kupoteza dhidi ya Ihefu Januari tatu mwaka huu, lakini tunafurahi kuwa wachezaji wetu wamerudi kwenye viwango vizuri hata kwenye mazoezi wanafanya wakiwa na hari na morali nzuri ambayo inaleta taswira njema kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar.”
KMC FC inakwenda kwenye mchezo wa mzunguko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikishika nafasi ya tisa mwa msimamo ikiwa na jumla ya alama 22.