Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage ameingilia kati sakata la Kiungo kutoka Visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ la kutakiwa kurejea Young Africans.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ ilitoa taarifa juzi Jumamosi (Januari 07) kwa kuthibitisha Fei Toto bado ni mchezaji halali wa Young Africans.

Kamati hiyo ilitoa taarifa ya maamuzi yake baada ya kusikiliza malalamiko yaliyowasilishwa na Uongozi wa Young Africans, kwa kumtuhumu Fei Toto kutoroka kambini na kuvunja mkataba pasina kufuata utaratibu.

Akizungumza kupitia Kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM mapema leo Jumatatu (Januari 09), Rage amesema TFF inapaswa kumuita Fei Toto na kumuuliza ni wapi anataka kucheza soka lake, baada ya kukiri wazo hana mahaba na Young Africans.

Amesema Kiungo huyo bado ni kijana mwenye umri mdogo anapaswa kupata usaidizi wa kina wa kisheria na sio kupelekeshwa kama taarifa ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilivyoeleza.

“Feisal aitwe na aeleze timu gani anataka kuichezea. Feisal ni mtoto mdogo na inatakiwa asaidiwe kwa kanuni ya Fair play.”

“Binafsi niliwahi kukutana na sekeseke kama la namna hii kwa mchezaji Mbuyi Twite, nilimsajili kabisa yule mchezaji, lakini akasajiliwa na Yanga pia, na kilichofanyika Mbuyi alichagua kuichezea Yanga na Simba tulitakiwa tulipwe fedha zetu.”

“Yanga walitulipa na wakatupa na fedha ya fidia. Kiukweli huwezi kumng’ang’ania mchezaji ambaye hayuko tayari kukutumikia ” amesema Rage

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilianza kusikiliza Malalamiko dhidi ya Feisal Salum Abdallah siku ya Ijumaa (Januari 06), huku kila upande ukiwakilishwa na Wanasheria wake, na Jumamosi (Januari 07) ilitoa taarifa ya kuendelea kumtambua Mchezaji huyo kuwa halali upande wa Young Africans.

Majaliwa ataka huduma bora za Afya kwa jamii
Waandishi mbaroni kwa kusambaza Video ya Rais akijikojolea