Kaimu Afisa Habari wa Azam FC Hashim Ibwe amemkingia kifua Mlinda Lango chaguo la tatu wa Azam FC Zuberi Foba, kufuatia lawama anazoendelea kutupiwa na baadhi ya Mashabiki wa Klabu hiyo ya Chamazi-Dar es salaam.

Foba alifanya makosa ya kushindwa kuulinda Mpira aliorudishiwa kipindi cha kwanza, na kusababisha Mshambuliaji Fancy Kazadi kufunga bao la kuongoza upande wa Singida Big Stars kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Mapinduni jana Jumapili (Januari 09), Uwanja wa Amaan Kisiwani Unguja ‘Zanzibar’.

Ibwe amesema alichokifanya Foba ni makosa ya kawaida ambayo yanaweza kumtokea Mlanda Lango yoyote duniani, hivyo si vyema kwa baadhi ya Mashabiki kumtupia lawama.

Amesema ingetokea Mlinda Lango huyo chipukizi angefanikiwa katika kusudio lake, kila shabiki angemsifu, lakini imekua tofauti na ndio maana kila mmoja amekua na sababu ya kulaumu.

“Kipa yoyote duniani anaweza kukosea na ndivyo ilivyotokea kwa Foba, binafsi siwezi kumlaumu kwa sababu ninajuwa halikuwa kusudio lake kufanya makosa yale.”

“Ninaamini kama angepatia kila shabiki angemsifia kwa kusema Kipa wa Azam FC ana uwezo wa kumfinya mtu ndani ya Box, kwa hiyo ningependa kuwaambia wanaomlaumu waache kwa sababu makosa hutokea na sio mara zote” amesema Ibwe

Azam FC imepoteza mchezo wa Nusu Fainali na kutupwa nje katika Kombe la Mapinduzi 2023 kwa kufungwa 4-1, matokeo anayoifanya Klabu hiyo kuwa klabu pekee iliyopoteza kwa idadi kubwa ya mabao kwenye Michuano hiyo.

Waandishi mbaroni kwa kusambaza Video ya Rais akijikojolea
Ajali yauwa 40, Rais atangaza siku tatu za maombolezo