‘Kuishiwa Mbinu’ kumetajwa kama sababu kubwa ya Uongozi wa Klabu ya Simba SC kuachana na Kocha Mkuu kutoka nchini Serbia Zoran Maki aliyeitumikia klabu hiyo kwa siku 56 tangu alipotangazwa kupitia Mkutano wa Waandidhi wa Habari Julai 12 mwaka huu 2022.
Uongozi wa Simba SC kupitia taarifa rasmi iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii jana Jumanne (Septemba 06), ilitangaza kuachana na Kocha Zoran kwa kufikia makubaliano ya kuvunjwa kwa mkataba baina ya pande zote mbili.
Mmoja wa mabosi wa klabu ya Simba ambaye hakutaka jina lake lianikwe hadharani, amesema wamefanyamaamuzi ya kuachana na Kocha huyo mwenye umri wa miaka 60, baada ya kujiridhisha kiufundi hana mbinu mbadala za kuivusha timu yao katika Michuano wanayoshiriki msimu huu.
“Timu imeonekana kucheza soka la kawaida ambalo haliendani na hadhi yetu, Simba SC sio timu ya kucheza soka la kujilinda muda wote, tulishazoea tukicheza soka la pasi na kushambulia.
“Pili, wachezaji kukosa furaha wakiwa kambini, mazoezini na katika michezo miwili ya ligi ambayo tumeicheza, licha ya kupata ushindi katika michezo hiyo.
“Hili la wachezaji kukosa furaha tumeona lingetuathiri katika ligi, kwani wachezaji ndio wanaopambana katika timu, hivyo tungeendelea kubaki naye basi angetuvurugia mipango yetu ya ubingwa.”
“Tatu, Timu kukosa utulivu inapokuwepo uwanjani ikicheza, hivyo hilo tumeliona tangu tukiwa katika pre season na kuamua kuchukua maamuzi magumu ya kuachana naye,” amesema bosi huyo.
Hata hivyo Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzales hakuwa tayari kuzungumza sababu hizo tatu, zaidi ya kuendelea kusisitiza wameachana na Zoran Maki na sasa wapo kwenye mchakato mfupi wa kumtangaza Kocha Mkuu mpya.
“Ni kweli tumeachana na Zoran, na mipango yetu kuwa na kocha wa mipango ya muda mrefu katika projekti yetu na sio kuwa na kocha mtalii.
“Na ninaamini mara baada ya taarifa hii, nitapokea maombi mengi ya makocha kutoka Ulaya kwa kutumia CV zao na sio Afrika. Katika ukanda huu Afrika wapo makocha wengi wa Afrika waliofanya vizuri na kufanya makubwa katika Kombe la Dunia.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika, wapo makocha watano Ukanda wa Afrika waliowezesha nchi mbalimbali kufuzu Kombe la Dunia ambao wanastahili kuja kuifundisha Simba na baadhi yao ni Jalel Kadri (Tunisia), Otto Addo (Mghana), Walid Regragui (Morocco), Aliou Cisse (Senegal) na Rigobert Song (Cameroon),” amesema Barbara.
Naye Meneja wa Habari wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema kuwa Haraka wameanza mchakato wa kumpata kocha mpya atakayekuja kuanza kazi kabla ya kuanza kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika Jumapili (Septemba 11).
Zoran Maki anakuwa kocha wa pili wa kigeni kuondoka katika majukumu yake tangu kuanza kwa msimu huu, akitanguliwa na Kocha Abdihamid Moallin kutoka nchini Marekani mwenye asili ya Somalia, aliyekua akikinoa kikosi cha Azam FC.