Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu amevuliwa rasmi kiti hicho, baada ya kuvunja taratibu mablimbali za Bunge ikiwemo kutohudhuria mikutano na vikao vya bunge bila kutoa taarifa.
Uamuzi huo umetangazwa na spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai wakati wa kuhitimisha mkutano wa kumi na tano, kikao cha hamsini na tano kilichoambatana na hoja ya kuahirisha bunge, ambapo amesema kuwa amemjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujaza nafasi hiyo.
”Napenda kuwafahamisha waheshimiwa wabunge kuwa kiti cha ubunge cha jimbo la Singida Mashariki kilichokuwa kinashikiliwa na Tundu Lissu kipo wazi na nimemjulisha Mwewnyekiti wa Tume ya Uchaguzi aendelee na taratibu za kukijaza,” amesema spika Ndugai
Aidha, amefafanua kuwa kutokana na Tundu Lissu, kushindwa kutoa taarifa kwa spika kwa muda wote ambao hayupo bungeni, pamoja na kutowasilisha tamko la mali zake anakuwa amevunja sheria ya uchaguzi.
”Kifungu cha 37, kifungu kidogo cha 3 cha sheria ya taifa ya uchaguzi sura ya 343, kinanitaka kumtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nini cha kufanya”.
Hata hivyo, spika ameongeza kuwa ni zaidi ya mwaka mmoja umepita ambapo Tundu Lissu amekuwa akionekana kwenye vyombo mbalimbali vya habari katika nchi tofauti, huku akiwa hajafika bungeni wala kutoa taarifa yoyote kwa spika au kupitia kwa uongozi wake kitu ambacho ni kinyume na Katiba.