Meneja wa Young Africans Hafidh Saleh amemaliza utata uliozuka hivi karibuni kuhusu kiungo Mshanbuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza.
Kiungo huyo kutoka nchini Burundi amekua na changamoto ya kutopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza tangu msimu huu 2021/22 ulipoanza mwishoni mwa mwezi Septemba, hali iliyozua maswali mengi na kuibua minong’ono kwa mashabiki.
Madai ya Ntibazonkiza kutoonekana kikosini yalikwenda mbali zaidi kwa kuhusishwa na matatizo binafsi na kocha mkuu Nasrideen Nabi, huku akiachwa katika safari ya mjini Songea mkoani Ruvuma ambapo Young Africans watacheza dhidi ya KMC FC kesho Jumanne (Oktoba 19), mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Meneja Hafidh Saleh amesema taarifa za kutoonekana kwa Ntibazonkiza katika safari ya Ruvuma zina sababu tofauti na ilivyodaiwa na wadau wa soka nchini.
Amesema Kiungo huyo ameachwa jijini Dar es salaam kufuatia kukosa sehemu kubwa ya mazoezi ya timu, kufuatia kuchelewa kurejea nchini akitokea kwao Burundi ambako aliitwa kwenye timu ya taifa ‘INTAMBA MURUGAMBA’.
“Saido hakufanya mazoezi na wenzake kwa kipindi kirefu, tangu amerudi kutoka kuitumikia timu yake ya taifa, hivyo kocha Nabi hajaona umuhimu wa kuja naye hapa Songea,” amesema Hafidh Saleh
Kuhusu maandalizi kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya KMC FC Hafidh amesema kila kitu kinakwenda vizuri na matarajio yao ni kupambana na kupata alama tatu za ugenini.
“Nyota wote walioondoka na timu wapo kwenye hali nzuri ya mchezo na wanawaheshimu wapinzani wao wamejiandaa kwa ajili ya kuendeleza mazuri waliyoyafanya katika michezo miwili ya mwanzo,” amesema.
Young Africans imeshacheza michezo miwili ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22 dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold FC na imeshinda bao 1-0 katika kila mchezo, huku ikijikusanyia alama 06.
KMC FC ambao watakua wenyeji katika mchezo wa kesho Jumanne (Oktoba 19) Uwanja wa Maji Maji, imecheza michezo miwili, ikipoteza dhidi ya Polisi Tanzania kwa mabao 2-0 kisha iliambulia sare ya 0-0 dhidi ya Coastal Union.