Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imeanza kusikilizwa leo mfululizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Kesi hii inasikilizwa mfululizo wakati tayari Oktoba 15, Sabaya alihukumiwa kifungo cha miaka 30 na wenzake wawili baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na makosa mawili ya kuunda kundi la kufanya unyang’anyi.

Washtakiwa wengine katika kesi inayosikilizwa kuanzia leo ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya

Katika kesi hii mshtakiwa Daniel Mbura ambaye alifungwa miaka 30 na Sabaya, hahusiki kwenye uhujumu uchumi.

Septemba 16, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Patricia Kisinda, Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka, alisema wanatarajia kuwa na mashahidi 20 na vielelezo 16 katika shauri hilo namba 27 la mwaka huu.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili Kweka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Felix Kwetukia na Wakili wa Serikali Neema Mbwana na Utetezi uliwakilishwa na mawakili Mosses Mahuna, Charles Adiel, Sylevster Kahunduka na Fridolin Gwemelo.

Kabla ya Wakili Kweka kuieleza Mahakama idadi ya mashahidi na vielelezo, waliwasomea upya mashtaka na maelezo ya awali, lakini washtakiwa hao walikana.

Tuhuma zinazomkabili Sabaya na wenzake ni kuongoza genge la uhalifu na kosa la tano ni utakatishaji fedha.

Washtakiwa wote saba wanadaiwa kupata Sh90 milioni huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Kosa la pili, tatu na nne Sabaya peke yake ameshtakiwa kwa makosa hayo ya kujihusisha na rushwa na anadaiwa kuchukua Sh90 milioni na matumizi mabaya ya ofisi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro.

Ilidaiwa mahakamani hapo Januari 22 mwaka huu kuwa, watuhumiwa hao wakiongozwa na Sabaya walikwenda katika gereji inayomilikiwa na mfanyabiashara Francis Mrosso, wakimtuhumu kufanya biashara bila kutoa risiti za kielektroniki huku wakidai anaingiza vifaa kutoka nje ya nchi pasipo kufuata taratibu za ulipaji kodi.

Ilidaiwa kuwa Sabaya alimtisha mfanyabiashara huyo wa eneo la Kwa Mrombo kuwa watamfungulia kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha haramu na kuwa walimtishia na kumlazimisha atoe Sh90 milioni ili awe huru.

Washtakiwa wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Simulizi:Ushuhuda wa Mchungaji kuhusu kupata waumini watiifu.
Sababu za Ntibazonkiza kuachwa Dar