Polisi Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania wamevamia mkutano wa ndani wa mbunge wa Hai, CHADEMA, Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni.
Polisi hao wakiongozwa na mkuu wa polisi wa Wilaya OCD, Lwele Mpina wamevamia mkutano huo leo Jumatatu ya Septemba 30, 2019 baada ya kuagizwa na mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.
Sabaya amethibitisha kutuma polisi hao akisema amefanya hivyo kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa Mbowe na viongozi wengine pamoja na wananchi, akisema kuwa hawana sababu ya taharuki kama raia wema.
”Mkutano wa chama cha siasa sio sendoff au harusi, Mkutano wa chama cha siasa polisi wana haki ya kuwepo. Hata mikutano ya CCM polisi wanakwepo, kuhakikisha kwamba watu waliopo pale wapo salama lakini watu waliopo pale hawasababishii uvunjifu wa amani wa watu wengine wa mazingira hayo, sababu rekodi yao inaonyesha siku zote mijadala ya siasa zao ni siasa za kugawa watu, ,sasa polisi watasaidai kuweka mstari” amesema Sabaya ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo.
Joel Nkya Kaimu ambaye ni Mwenyekiti Wilaya ya Hai CHADEMA, nae amesema ”kama wameona ni njia nzuri ya kuhakikisha usalama upo hatuwazuii kwasababu tumeendelea kufanya vyetu kwa sababu hatuna siri, mambo yetu ni wazi” .
Aidha, baada ya kuwasili kwa askari hao Mbowe na viongozi wenzake walisalimiana nao na kuendelea na kikao chao ambapo katika salamu zao polisi walisikika wakisema wapo pale kwa kuimarisha ulinzi tu na si sababu nyingine.