Mtu mmoja anayedaiwa kuwa ni jambazi ameuawa kwa kupigwa risasi  katika majibizano ya risasi na Jeshi la  Polisi.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 7:30 mchana eneo la Ilala Boma Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi wa Ilala, Zuberi Chembela amesema kuwa mhalifu huyo alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu na kwamba alianza kufukuzwa kuanzia eneo la Magomeni.

”Hilo tukio naomba mmpigie Afande Mambosasa kwasababu huyo mhalifu alikuwa anakimbizwa kutokea Magomeni, kwahiyo alivyofika hapo akazingirwa na ndipo kikatokea hicho kilichotokea na hilo tukio limehusisha mikoa miwili, Ilala na Kinondoni hivyo ni vyema mkamtafuta Mambosasa atalizungumzia vizuri zaidi”, amesema Chembela.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP Lazaro Mambosasa, amethibitisha kupokea taarifa ya tukio hilo akisema,

”ni kweli tukio hilo limetokea, askari wetu walikuwa wanapambana na huyo jambazi, alikuwa anafuatiliwa na hiyo milio iliyosikika walikuwa wanapambana naye na tumefanikiwa kupata Bastola moja”, amesema SACP Mambosasa.

Aidha, Kamanda Mambosasa amesema kuwa atatoa undani wa tukio hilo, punde tu atakapopokea vielelezo vyote.

Sabaya atuma polisi kuzingira mkutano wa Mbowe
Rais Magufuli aonya, aongeza siku 7 za msamaha watuhumiwa uhujumu uchumi