Matumaini ya Kiungo kutoka nchini Mali Sadio Kanoute kutumika kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Jwaneng Galaxy yanaendelea kuongezeka kambini kwa Mabingwa wa Tanzania Bara.
Kanoute alikua nje kwa zaidi ya majuma mawili akiuguza jeraha alilolipata kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans, lakini tangu mwishoni mwa juma lililopita amekua akionekana kwenye mazoezi ya kikosi cha Simba SC ambacho kinajiandaa na Mshike Mshike wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kocha Mkuu wa Simba SC Didier Gomes amesema maendeleo ya kiungo huyo aliyesajiliwa miezi miwiwli iliyopita klabuni hapo anaendelea vizuri na amekua akifanya viziri mazoezi tangu aliporejea.
Gomes alisema: “Kama mnavyojua tulimkosa Kanoute katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara kutokana na majeraha, lakini tunashukuru kwa sasa amepona kwa asilimia kubwa.
“Tunamuhitaji katika mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Galaxy ili kupata matokeo chanya, kwa kuwa ni mchezaji muhimu kwetu ambaye tayari ameonesha wazi kwa kila mtu kuwa ni miongoni mwa viungo bora kwa sasa kutokana na uwezo mkubwa alionao.”
Oktoba 17, mwaka huu, Simba SC itapambana na Jwaneng Galaxy , kisha kurudiana Oktoba 22, ambapo mshindi wa jumla anaenda hatua ya makundi huku atakayepoteza atangukia kwenye michezo mtoano ya Kombe la Shiriksiho dhidi ya walioshinda michezo ya Michuano hiyo kutafuta nafasi ya kutinga makundi.