Kiungo Kutoka nchini Mali Sadio Kanoute hatokua sehemu ya kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kitakachoivaa Namungo FC kesho Jumanne (Mei 03) mkoani Lindi.
Kikosi cha Simba SC leo Jumatatu (Mei 02) kimeweka kambi Mtwara baada ya kuwasili mkoani hapo, ikitokea jijini Dar es salaam mapema asubihi.
Meneja wa Habari na mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema kiungo huyo amebaki Dar es salaam, kufuatia majeraha aliyoyapata kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans Jumamosi (April 30).
Ahmed amesema kiungo huyo alitarajiwa kufanyiwa vipimo leo Jumatatu, ili kufahamu ukubwa wa jeraha hilo ambalo lilimkosesha nafasi ya kuendelea na mchezo wa Young Africans.
“Tumekuja na kikosi chetu chote kasoro Sadio Kanoute, amebaki Dar es salaam kutokana na jeraha alilolipata kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans, leo atakwenda kufanyiwa vipimo ili kujua ukubwa wa jeraha linalomsumbua.”
“Tunaamini akishafahamu ukubwa wa jeraha, itafahamika atakua nje kwa muda gani kwa ajili ya kufanyiwa matibabu, na sisi kama viongozi tunamtakia kila la kheri ili apone haraka na kurudi kwenye majukumu yake.”
“Mashabiki wa Simba waendelee kuwa watulivu kuhusu hali ya Sadio Kanoute, kwa sababu tunaamini mambo yatakua sawa na tutawafahamisha kila kitu kuhusu hali yake.” amesema Ahmed Ally
Simba SC ipo nafasi ya pili katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 42, huku ikiachwa kwa tofauti ya alama 13 dhidi ya vinara Young Africans yenye alama 55.
Namungo FC inashika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 29 sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya nne, kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.