Mtayarishaji wa filamu na makala kutoka Hollywood, John Feist, ambaye ndiye mtayarishaji maalumu wa filamu za ‘Royal Tour’ zote zilizofanyika katika mataifa mbali mbali duniani ikiwamo Tanzania, amezichambua filamu za Tanzania na kuweka wazi kuwa ipo njia mbadala inayoweza kutumika kuzifanya ziwe filamu bora.

John Feist amesema ikiwa Tanzania inataka kuwa ‘SwahiliHood’ kuna jinsi ya kufanya maboresho katika uandaaji wake.

Akizungumza katika Semina iliyofanyika jijini Dar es salaam, Feist amekiri kupata wasaa wa kuangalia filamu kadhaa za Tanzania zilizopata nafasi katika mtandoa wa Netflix na kuona kuna changamoto zinazotakiwa kufanyiwa kazi.

“Sijui kazi zenu nyingine lakini hata zile nilizopata muda wa kuzitazama, hasa zilizokubaliwa Netflix, ni nzuri lakini bado kuna shida ya uandishi na muunganiko wa hadithi,” alisema Feist.

“Viwango vya Hollywood, hoja sio picha nzuri au urefu wa filamu, wenzenu kule, na hata makampuni ya kufadhili filamu, wanaangalia sana kisa na mtiririko wa hadithi yako, Nitasaidia kidogo eneo hili, nitakuwa mtaalamu wenu lakini kwanza someni hiki.” aliongeza.

Feist ametoa kitabu cha jinsi ya kuandika miswada ya filamu kinachotumika Hollywood, na amedokeza kuwa ni muhimu uigizaji wa filamu za Tanzania uzingatie utofauti kati ya Filamu na Riwaya.

“Filamu inatakiwa action, novel ina maelezo marefu sana. Sasa nimeona filamu zenu zina maelezo sana bila vitendo lakini pia zinakosa mtiririko zinaisha ghafla kabla haujaelewa mkasa umeishaje,” alisema.

Feist amewatoa shaka waandaaji wa filamu nchini na kuwapa muongozo wa jambo la kufanya ili kufikia hatua ya kupata ufadhili wa maandalizi ya filamu nchini.

“changamoto ya ufadhili wa filamu Tanzania itakwisha iwapo miswada na hadithi vitazingatiwa na kuhakikisha vimekaa sawa na kinachohitajika sokoni, ni rahisi kufadhili filamu nzuri kuliko iliyoharakishwa,” ameongeza Feist.

Feist aliyazungumza hayo alipohudhuria kwenye semina maalumu na watayarishaji, wasanii pamoja na wadau mbali mbali wa sekta ya filamu Tanzania mapema mwezi Aprili, 2022 katika ukumbi wa JNICC Dar es salaam.

John Feist pia ni muandishi nguli wa scripts, na mshindi wa tuzo ya Emy aliyoipata kutokana na kuhusika katika utayarishaji wa filamu maaarufu Survivor.

Sadio Kanoute kuikosa Namungo FC
Ukweli wa Drama za Harmonize na Omondi wathibitika kuishia Mei 20