Kwa mara ya Kwanza Mshambuliaji wa FC Bayern Munich y7a Ujerumani Sadio Mane, ametuma ujumbe kwa Mashabiki walioguswa na hatua ya kuumia kwake, hali ambayo imepelekea kuzikosa Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini QATAR.
Mane alipata majeraha ya mguu majuma mawili yaliyopita akiwa katika jukumu la kuitumikia klabu yake FC Bayern Munich ya Ujerumani, siku chache kabla ya kuitwa kwa kikosi cha Senegal kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia.
Mshambuliaji huyo alikua kimya kwa kipindi cha majuma mawili alipoanza kujiuguza maumivu wa Mguu, huku wengi wakiumizwa na taarifa ya mwisho iliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini Senegal kuwa, hatokuwa sehemu ya kikosi cha nchi hiyo kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Mane ametumia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii kuwashukuru Mashabiki wote waliomtumia ujumbe wa Pole na Kheri katika kipindi chote ambacho atakua anajiuguza jeraha lake la mguu.
Pia Mshambuliaji huyo ameitakia kila la kheri timu yake ya taifa ya Senegal, ambayo leo Jumatatu (Novemba 21) itacheza mchezo wake wa kwanza katika Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi.
“Nataka kuchukua fursa hii kuwashukuru wale wote ambao mmenitumia ujumbe wa kunipa pole na kunitakia kheri kufuatia jeraha langu.”
“Jumatatu hii (leo) nchi yetu pendwa itashiriki Kombe la Dunia Qatar 2022. Nina hakika Simba itacheza kila mchezo kama fainali. (Wachezaji) watapambana kama timu” ameandika Sadio Mane.
Mchezo huo wa Kundi A umepangwa kuanza majira ya saa moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki, mchezo ambao utaunguruma katika Uwanja wa Al Thumama, mjini Doha.
Mwamuzi Wilton Sampaio kutoka nchini Brazil amepewa jukumu la kusimamia sheria 17 za mchezo wa Soka katika dakika 90, ambazo zitashuhudia miamba hiyo ya Afrika ikizisaka alama tatu muhimu dhidi ya The Orange.
Tayari mchezo mmoja wa Kundi A umeshapigwa kati ya Wenyeji ‘QATAR’ waliokubali kulala mabao 2-0 dhidi ya Ecuador jana Jumapili (Novemba 20), katika Uwanja wa Al Bayt Stadium, mjini Al Khor.