Rais Guinea ya Ikweta, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo (80), atarajiwa kuendelea kuitawala nchi hiyo baada ya uchaguzi wa Novemba 20, 2022, huku wapinzani wakilalamika kuwa ulitokea udanganyifu na ukiukaji wa sheria, katika uchaguzi huo.

Teodoro Obiang, ametawala kwa muda wa miaka 43 katika katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta, akiingia madarakani mwaka 1979 baada ya kuuangusha utawala wa rais wa kwanza wa nchi hiyo iliyopata uhuru wake kutoka kwa Wahispania 1968.

Katika uchaguzi uliofanyika hapo jana Novemba 20, Obiang anatarajiwa kupata zaidi ya asilimia 95 ya kura na hivyo kuendelea na muhula wa sita, huku Msimamizi wa vituo vya uchaguzi Maria Amparo Se Obama, akieleza kuwa zoezi la upigaji kura lilikwenda salama.

Rais Guinea ya Ikweta, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo (80). Picha ya The Independent.

Mchakato wa kuhesabu kura unaendelea na matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani yanatarajiwa kutangazwa katika siku chache zijazo huku mmoja wa wagombea wawili wa pekee waliochuana na rais Obiang katika kinyang’anyiro cha urais, Andres Esono akisema anachokifanya kiongozi huyo ni ulaghai mbaya kuliko wa hapo awali.

Esono, amewaambia waandishi wa habari kuwa chama chake kimepokea malalamiko kutoka katika sehemu mbalimbali kwenye taifa hilo la Afrika ya Kati kwamba wapiga kura walilazimishwa kupiga kura zao hadharani badala ya kupiga kwa siri.

Vyama 14 vya upinzani nchini humo vilijiunga kwenye muungano na chama tawala, ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu yanakilaumu kwa ukiukaji wa haki za binadamu, vitisho, kuwawinda wapinzani, utesaji, kupotezwa kwa watu na ufisadi.

Mgombea wa Chama cha upinzani, Andres Esono Ondo anadai uchaguzi uligubikwa na udanganyifu. Picha ya El Diario.

Hata hivyo, serikali ya Obiang pia imelaumiwa kwa kuwaandama wanaodaiwa kupanga mapinduzi waliokimbilia katika nchi nyingine na kuwarudisha kwa nguvu nchini Guinea, ambapo walihukumiwa kifo.

Aidha, Obiang amesema ana matumaini ya chama chake cha PDGE kushinda tena katika uchaguzi huo mara baada ya kupiga kura pamoja na mkewe, Constancia Mangue de Obiang ambapo katika chaguzi zilizopita, hakuwahi kupata chini ya asilimia 90 ya kura.

Licha ya utajiri wake wa mafuta na gesi, taifa la Guinea ya Ikweta limo katika hali ya kushangaza ambapo pengo ni kubwa kati ya tabaka la watawala na idadi kubwa ya watu wanaoishi, hasa kwa kutegemea kilimo cha kujikimu.

Mtoto wa rais Obiang, Teodoro Nguema Obiang Mangue, ‘Teodorin’ ndiye Makamu wa Rais wa Guinea ya Ikweta. Picha ya AFP.

Mtoto wa rais Obiang, anayeitwa Teodoro Nguema Obiang Mangue, maarufu kama Teodorin, anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali za serikali, huku baba yake akimpandisha cheo na kumtangaza kuwa makamu wa rais na tayari wadadisi wametabiri kwamba anaandaliwa kwa ajili ya kumrithi baba yake.

Mapema 2021, Mahakama ya Ufaransa ilimuhukumu Teodorin kwa makosa ya ufujaji wa pesa na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za umma na alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu na faini ya Euro milioni 30 huku Mahakama hiyo ikiagiza kukamatwa mali zake za nchini Ufaransa zenye thamani ya mamilioni ya Euro.

Rais wa zamani wa Marekani kuchunguzwa
Sadio Mane awatumia ujumbe mashabiki