Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC Haji Sunday Ramadhan Manara amemuahidi Mwanachama wa Young Africans Mzee Mpili, kumpambania ili apate tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi Mkoani Kigoma, kwa ajili ya kushuhudia mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC).
Simba na Young Africans zitakutana fainali ya ASFC Julai 25 katika Uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma, baada ya kushinda michezo yao ya nusu fainali dhidi ya Azam FC na Biashara United Mara iliyochezwa mwishoni mwa mwezi Juni kwenye mikoa ya Ruvuma na Tabora.
Manara amempa ahadi hiyo Mzee Mpili, alipomkaribisha nyumbani kwao jana Jumatano Jioni kwa ajili ya kumkabidhi Shilingi Milioni Moja aliyomuahidi, kabla ya mchezo wa Simba na Young Africans uliochezwa Jumamosi (Julai 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Manara amesema amemuhakikishai Mzee Mpili kuwa atazungumza na Injia Hersi Said ili kumuombea tiketi ya kwenda Kigoma kushuhudia mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka Tanzania.
“Nitaongea na Hersi Said ili akupatie tiketi ya kwenda Kigoma Mzee, lazima uende ukashuhudie mchezo wa fainali ambao kila mmoja anausubiri kwa hamu kubwa.” alisema Manara kumwambia Mzee Mpili.
Katika hatua nyingine Mzee Mpili amemshukuru Haji Manara kwa kutimiza ahadi yake ya kumpa Shilingi Milioni Moja kama alivyokua ameahidi kabla ya mchezo wa Jumamosi (Julai 03).
Manara alitoa ahadi hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii (Instagram), ambapo alimuahidi mzee huyo endapo Young Africans ingeifunga Simba angempatia fedha hizo, na ndivyo ilivyokua.
“Ninakushuru sana Babu Haji kwa kutimiza ahadi yako, nimefurahi nimekuja nyumbani kwao hapa na umenitimizia ulichoniahidi, mungu akubariki sana.” alisema Mzee Mpili.