Vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC wanaamini kikosi chao kina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kuwa na safu imara na nzuri ya ushambuliaji.
Azam FC wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 12, baada ya kushinda michezo minne waliocheza, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Simba SC na Young Africans wenye alama 10 kila mmoja.
Kocha msiadizi wa Azam FC Vivier Bahati amesema safu yao ya ushambuliaji imeonyesha ukomavu wa kupambana tangu walipoanza msimu huu, ambao amekiri una changamoto kubwa ya ushindani.
Kocha Bahati amesema kutokana na mazingira ya changamoto ya ushindani, wamewaandaa wachezaji wao wanaocheza nafasi ya ushambuliaji ili kupambana katika kila mchezo na kupata matokeo chanya.
“Msimu huu tuko kwenye mbio za ubingwa, tunajivunia safu bora ya washambuliaji tuliyokuwa nayo, kila mshambuliaji atakayecheza anaweza kufunga na kuibuka na ushindi, hii inatujenga na kutuweka mahali salama,” amesema Bahati.
“Tumejipanga kuleta ushindani mkubwa, ukiangalia safu ya ushambuliaji imekuwa na mabadiliko tofauti na msimu uliopita, imani yetu tunapambana kutafuta matokeo mazuri katika kila mechi tunazocheza za nyumbani na ugenini pia.” Amesema Vivier.
Azam FC wamerejea jijini Dar es salaam wakitokea mkoani Rukwa walipocheza dhidi ya Tanzania Prisons mwishoni mwa juma lililopita, na mwishoni mwa juma hili watacheza dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kagera Sugar.