Kiungo wa Klabu ya Simba SC Said Hamis Ndemla amekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zilizoeleza mustakabali wake mara baada ya mkataba wake utakapofikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.
Ndemla amekua katika vichwa vya habari vya magazeti na mitandao ya kijamii kila kukicha kutokana na changamoto inayomkabili ndani ya kikosi cha Simba, huku mkataba wake ukielekea ukingoni.
Kiungo huyo ambaye amekuwa na Simba tangu akiwa kijana mdogo, amekanusha uvumi huo kwa kusema hakuzungumza na chombo chochote cha habari, wala kuandika lolote katika mitandao ya kijamii jana jumatatu.
“Hakuna kitu nilichoposti siku ya leo (jana), wala kitu chochote nilichongea mwezi huu.” Amekanusha Said Ndemla, kiungo wa Simba.
Hatua ya kukanusha huko, imetokana na taarifa zilizoenea ambazo zilibebwa na kichwa cha habari: Acha nikae benchi tu siondoki Simba “Ndemla”.
Katika taarifa hizo Ndemla alidaiwa kuwalaumu waandishi wa habari kwa kuwa sehemu ya kumshurutisha aondoke Simba SC, pindi mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa hiyo ilionyesha nukuu ya maneno ambayo yalidaiwa kusemwa na kiungo huyo: “Sijawasahau waandishi wa Habari kanjanja walivyo waharibia maisha rafiki zangu vijana wenzangu. Waandishi hao hao kanjanja wamenigeukia na mimi wamekua wakikesha wakiandika habari zangu niondoke simba kwa ajiri ya mapenzi yao.”
“Nasema hivi nitaondoka Simba kwa matakwa yangu si kwa kulazimishwa. Mnawakumbuka Edo Christopher? Chanongo je? Singano nae? Hawa wote waliondoka Simba kwa shinikizo la waandishi kanjanja, Kwa Ndemla mmekwama nina miaka 24 kudanganyika siwezi acheni nikae benchi mbona nyie hata benchi hampo?”
Mbali na kukanusha huko Ndemla akaeleza mipango na matarajio yake ndani ya kikosi cha Simba SC.