Wakala wa Kiungo Mshambuliaji kutoka Burundi na klabu ya Young Africans Said Ntibazonkiza, ameikana klabu ya RS Berkane ya Morocco ambayo inatajwa kumuwania mchezaji huyo.
Ntibazonkiza ambaye mpaka sasa ameonesha kiwango kikubwa kwenye kikosi cha Young Africans, anahusishwa na mpango wa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, baada ya mkataba wake kufikia ukingoni.
Wakala wa kiungo huyo amethibitisha kupokea ofa kutoka kwenye moja ya klabu kubwa barani Afrika, ambayo hakuwa tayari kuitaja.
Amesema taarifa za Ntibazonkiza, kuwaniwa na RS Berakane hazina ukweli, lakini uhakika ni kwamba mchezaji wake yupo katika mazingira ya kuondoka Young Africans, endapo mambo yatakaa sawa na klabu iliyotuma ofa ya kutaka kumsajili.
Hata hivyo Wakala huyo amesema bado hajakutana na Viongozi wa Young Africans ili kufahamu mustakabali wa Ntibazonkiza, na atakapofanya hivyo atakua na jibu sahihi kama Kiungo huyo ataondoka Tanzania mwishoni mwa msimu huu ama la.
“Bado sijakaa na Young Africans kuzungumza nao kama tunaendelea nao au la, ila tayari tuna ofa nyingi kutoka nje ya nchi, hivyo baada ya kumalizana na Young Africans nitajua wapi mteja wangu anaelekea.” amesema Wakala huyo
Saido alisajiliwa Young Africans wakati wa Dirisha Dogo la Usajili msimu uliopita (2020/21), baada ya kuonyesha uwezo mkubwa alipoitumikia timu yake ya Taifa kwenye mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Katika mchezo huo Burundi iliifunga Tanzania bao 1-0, ambalo lilikwamishwa wavuni na Ntibazonkiza baada ya kupiga shuti kali lililomshinda Mlinda Lango David Kissu.