Mamlaka za Usalama jijini Conakry nchini Guinea, imewakamata wanachama watatu wa Chama cha Upinzani cha FNDC, akiwemo mratibu wa kitaifa, Fonike Mangue anayejulikana pia kama Oumar Sylla.
Tukio la kukamatwa, limetokea wakati Viongozi hao wakiwa kwenye kikao na Wanahabari kilichofanyika katika Makao Makuu ya Muungano huo, unaolenga kurejesha utaratibu wa Katiba ya nchi inayodaiwa kuwa na mapungufu.
Muungano huo wa Kitaifa wa Kutetea Katiba, FNDC hivi karibuni umetishia kuandamana dhidi ya utawala wa Kijeshi unaoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya, uliochukua nafasi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo Alpha Condé.
Wakizungumza baada ya kukamatwa kwa watu hao, Viongozi waliosalia wa Muungano huo wameahidi kuendelea kupigania demokrasia.
“Hakuna kurudi nyuma, tumeamua kupigania kurejea kwa utaratibu wa kikatiba, na hili lazima litimie kwa amani tu lakini hivi vitisho havitatukatisha tamaa,” amesema afisa wa operesheni wa FNDC, Ibrahima Diallo.
Kwa upande wake mjumbe wa FNDC, Abdoulaye Oumou Sow amesema, “sasa tunapoona hatupo tena katika utawala wa sheria, hakuna tena mlango wazi wa mazungumzo, tunaona tuko kwenye udikteta, tunaenda kupigana na mapambano haya yataongozwa na watu wa Guinea.”
Muungano wa FNDC, ulipanga miezi kadhaa ya uhamasishaji dhidi ya Rais wa zamani Alpha Condé aliyeondolewa madarakani Septemba, 2021 huku Mkuu wa kikosi cha kijeshi, Kanali Mamady Doumbouya akiahidi kukabidhi madaraka kwa raia waliochaguliwa ndani ya miaka mitatu.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ilikataa utaratibu huo katika mkutano uliofanyika jijini Accra Jumapili Julai 3, 2022, bila kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Guinea.