Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal na Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Pape Ousmane Sakho, amefichua siri ya kikao cha Wachezaji wa klabu hiyo, baada ya kurejea jijini Dar es salaam Jumanne (Machi 22), wakitokea Conotou-Benin.

Simba SC ilicheza dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast Jumapili (Machi 20), na kuambulia kisago cha mabao 3-0, ambacho kimeiweka njia panda ya kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Sakho ambaye alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu amesema baada ya kurejea jijini Dar es salaam wachezaji wote wa Simba SC wamefanya kikao na kukubaliana namna watakavyoikabili USGN ya Niger katika mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ utakaounguruma Jumapili (April 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Tumekutana kama wachezaji na niseme Simba hatujatoka katika mashindano ila tumepoteza moja ya mchezo na tumeumia kwa matokeo yale,”amesema Sakho ambaye michezo ya wekundu hao nyumbani ametupia kila mchezo bao moja tena makali.

“Tukirudi kambini kama wachezaji tumekubaliana kwamba tunatakiwa kurudisha heshima yetu kupitia mchezo wa Gendarmerie ‘USGN’ naiona Simba SC ikifuzu tena kupitia uwanja wa nyumbani,” aliongeza kiungo huyo.

Tayari Simba SC imeshaanza kuuza tiketi za mchezo huo utakaopigwa saa moja usiku, huku Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ likitoa kibali cha mashabiki 35,000 wataoshuhudia mchezo huo wakiwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kabla ya mchezo huo wa mwisho, Msimamo wa ‘Kundi D’ unaonyesha ASEC Mimosas inaongoza ikiwa na alama 09, ikifuatiwa na RS Berkane yenye alama 07 sawa na Simba SC huku USGN ikishika nafasi ya nne ikiwa na alama 05.

Franco Pablo Martin: Siku saba zinatosha
Kocha Dodoma jiji aihofia Tanzania Prisons