Aliyekuwa Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ wa Simba SC Pape Ousmane Sakho amemshukuru Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, Sadio Mane kwa kumtafutia timu nchini Ufaransa.
Sakho aliyejiunga na timu ya Sportive Quevillaise-Rouen Metropole ya Ligi Daraja la Pili Ufaransa, aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter akifichua kuwa Mane alimsaidia kujiunga na timu hiyo.
“Asante kaka Sadio Mane kwa kufanikisha mpango wa mimi kucheza Ufaransa. Siku zote utabaki kuwa mfano mzuri kwangu na kuwa kwenye kumbukumbu za maisha yangu,” ameandika Sakho.
Sakho walikutana na Mane kwa mara ya kwanza wakati akipokea tuzo ya bao bora la michuano ya ngazi ya klabu ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) akifunga bao hilo dhidi ya Asec Mimosas, Mane akitangazwa kuwa mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2021.
Aidha, Sakho amesema ni suala gumu kuagana na klabu ya Simba SC na haukuwa uamuzi rahisi kuondoka kwenye klabu hiyo aliyosema itaendelea kuwa kwenye kumbukumbu yake kwenye maisha yake ya soka.
“Sio rahisi kusema kwa heri. Ulikuwa uamuzi mgumu kuchukua, lakini soka ndivyo lilivyo.
“Kitu muhimu kwangu ni kwamba tayari tumekuwa familia na wakati wote mliniunga mkono.