Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amewaasa wawekezaji na wafanyabiashara nchini kuibua fursa zinazofungamana na sekta ya madini ili kukuza uchumi wa Taifa
Ametoa rai hiyo leo Februari 22, 2021 wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa uwekezaji uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano Mwalimu Nyerere JNICC jijini Dar es Salaam huku kauli mbiu ikiwa ni Sekta ya Madini kwa Uchumi Imara na Maendeleo Endelevu.
Aidha, amewaomba washiriki wa Mkutano huo kujadili namna ya kufanya sekta hiyo izidi kukuza uchumi wa nchi na kuwahimiza kufuata sheria za nchi katika utekelezaji wa shughuli zao.
Sambamba na hayo Mama Samia amewataka washiriki wa mkutano huo kueleza changamoto wanazozipata katika sekta ya madini ili serikali izifanyie kazi.
Ameongeza kuwa sekta ya madini imeendelea kutoa mchango mkubwa katika mapato ya nchi na kwamba fedha zilizokusanywa kutokana na shughuli za madini zimekuwa zikioongezeka katika miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2015 / 2016 hadi 2019 / 2020.
Katika Mkutano huo Samia amebainisha kuwa serikali imepanga kufikia mwaka 2025 sekta ya madini iwe imeichangia asilimia 10 ya pato la taifa.