Wananchi wametakiwa kuwafichua watu wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto kijinsia ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Juni 17, 2017 Jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya Shule ya msingi Kinyerezi vilivyopo jijini humo.
Samia amesema watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji wa watoto wapo miongoni mwa jamii hivyo ni jukumu la Serikali, walezi na wazazi kuwafichua watenda maovu hao ili kukomesha vitendo hivyo na kuwafanya watoto waishi kwa amani nchini.
”Katika kukabiliana na hali hiyo, nimeviagiza vyombo vya dola kutofumbia macho vitendo hivyo pindi wanapopata taarifa za matukio ya udhalilishaji wa watoto na badala yake wachukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya,” alisema Mhe. Samia.
Amesema kuwa kufanya hivyo kutawasaidia watoto kuwa salama katika mazingira ya nyumbani hata wakiwa mashuleni kwani watu wabaya wanaofanya vitendo hivyo watawajibishwa kulingana na matendo maovu wanayoyafanya watoto.
Pia, ametoa wito kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kote nchini kuwapatia taarifa Walimu wao na Polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.