Wizara ya ulinzi ya Urusi imedai kuwa huenda jeshi la nchi hiyo lilifanikiwa kumuua kiongozi mkuu wa kundi la magaidi linalojiita Islamic States of Iraq and Syria (ISIS), Bakr al-Baghdadi katika shambulizi la anga lililotekelezwa mwezi uliopita nchini Syria.

Wizara hiyo imeeleza kuwa ilitekeleza shambulizi kali la anga Mei 28 mwaka huu kwenye mji wa Raqqa unaoshikiliwa na ISIS, ambapo kulikuwa na taarifa za kufanyika kwa kikao cha viongozi wa kundi hilo la kigaidi na inasadikika kuwa Al Baghdadi pia alihudhuria.

“Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimekuwa zikithibitishwa kupitia njia mbalimbali, kiongozi wa ISIS, Abu Bakr al-Baghdadi pia alihudhuria mkutano huo na aliuawa kutokana na matokeo ya mashambulizi ya anga tuliyoyafanya,” imeeleza taarifa ya wizara ya ulinzi ya Urusi.

Kwa upande wa Marekani ambao pia wanapambana na kundi hilo, wameanzisha uchunguzi wa kijesusi kufahamu kama kiongozi huyo pia aliuawa lakini wamethibitisha kuwa Urusi ilifanya shambulizi hilo.

Taarifa ya Urusi imeeleza kuwa katika mkutano huo, viongozi wa juu wa ISIS walikuwa wanajadili namna ya kuondoka katika mji huo. Imeongeza kuwa karibu makomando 30 na wanajeshi wa kawaida 300 wanaofanya kazi kama walinzi wa viongozi hao walikuwa sehemu ya mkutano huo na huenda waliuawa.

Hata hivyo, kumewahi kuwa na taarifa za kifo cha kiongozi huyo wa ISIS, taarifa ambazo baadae zilikuja kukanushwa na kuthibitika kuwa hazikuwa za kweli.

Samia awataka wananchi kufichua wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto
Makomando 7 wa Marekani wapotea baada ya meli ya kivita kugongwa Japan