Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia
Suluhu Hassan anatarajia kumwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye Mkutano wa dharura wa pamoja baina ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Organ Troika (Botswana, Malawi na Zimbabwe), na nchi zinazochangia vikosi vya ulinzi na amani vya Umoja wa Mataifa, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC.
Akithibitisha kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo utakaofanyika tarehe 28 Novemba 2020, mjini Gaborone, Botswana Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo utaongozwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akimwakilisha rais Magufuli.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, mkutano huu utatanguliwa na mkutano
wa Maafisa Waandamizi/Makatibu Wakuu wa Asasi ya SADC ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama na kufuatiwa na mkutano wa dharura wa kamati ya Mawaziri wa Asasi ya SADC ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama tarehe 26 Novemba 2020.
“Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda ya SADC na kuweza kuona changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kupata majibu ya kutatua changamoto hizo,” amesema Prof. Kabudi.
Makamu wa Rais ataambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Kabudi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi Dkt. Faraji Mnyepe pamoja na Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Ushirikiano wa Kikanda na Mratibu Kitaifa wa Masuala ya SADC, Bibi Agnes Kayola.
ASASI ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama (Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inawajibika kukuza amani na usalama katika eneo la SADC na pia ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi Wanachama mwongozo kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.