Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa sampuli ya mkojo wa msanii Agnes Gerald maarufu kama Deal ama Masogange (28) umebainika kuwa na dawa ya kulevya aina ya heroin na Oxazepam.
Akitoa ushahidi huo leo Jumatano mbele ya hakimu mkazi, Wilard Mashauri ameiambia mahakama kuwa mnamo Februari 15 2017 Askari wawili kutoka jeshi la polisi, Koplo Sospeter na WP Judith walimfikisha Masogange Ofisini kwake kwa lengo la kumfanyia vipimo vya mkojo.
Mkojo wa Masogange ulipimwa na mkemia mkuu na kubainisha kuwa unachembechembe za dawa za kulevya aina ya heroin ambazo kitaalamu zinajulikana kama Diacet Imophine.
Mkemia mkuu ameeleza kuwa uchunguzi zaidi ulifanywa kwenye sampuli ya mkojo wa Masogange na kubainisha kuwa una chembechembe nyingine ya dawa za kulevya aina ya Oxazepam.
Maelezo hayo yametolewa na aliyekuwa shahidi, Willbard Mashauri akiongozwa na wakili wa serikali Constatine Kakula wakidai kuthibitisha uwepo wa dawa za kulevya katika mkojo wa mwanadada Masogange kama ilivyobainishwa na Mkemia Mkuu.
Hata hivyo mawakili Nehemia Nkoko na Reuben Simwanza wamesimamia kidete kuhusu kukanusha taarifa hizo kuhusu mkojo wa Masogange kubainika kuwa na chembechembe zenye dawa za kulevya wakiomba mahakama kutopokea taarifa hizo wakidai hazijakidhi vigezo na sheria.
Nkoko amedai kuwa sheria hazikufuatwa kwani tamko la kuruhusu vipimo lilitakiwa kutoka mahakamani na sio Polisi.
”Ripoti ipo kinyume na sheria, mahakama ina njia moja tu nayo ni kuikataa na sio kuikubali. Sheria ipo wazi, ” tunaomba mahakama ikubali pingamizi letu na kukataa kupokea taarifa hiyo” amesema Nkoko.
Hakimu mashauri amehairisha shauri hilo hadi Agosti 28 kulitolea maamuzi aidha kupokea taarifa hiyo au kutokuzipokea.
Masogange amefikishwa mahakamani hapo akidaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya heroin kati ya februari 7 na 14 mwaka, na kutolewa kwa dhamana.