Makocha Samson Siasia na Winfried Schafer wanatajwa kuwa katika ushindani wa hali ya juu wa kuwania ukuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Rwanda.
Schafer aliiongoza timu ya taifa ya Cameroon mwaka 2002 na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika, huku Siasia ambaye aliwahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria anachagizwa na sifa za kuinoa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ya nchi hiyo na kuiwezesha kutwaa medali ya shaba wakati wa michuano ilimpiki mwaka 2016.
Kocha kutoka nchini Ubelgiji Paul Put, ambaye aliinoa Burkina Faso katika fainali za AFCON za mwaka 2013 na Georges Leekens, ambaye alitangaza kujiuzulu kukinoa kikosi cha Algeria mwezi uliopita, ni miongoni mwa walioomba nafasi ya kukifundisha kikosi cha Rwanda.
Shirikisho la soka nchini Rwanda (FERWAFA), limetoa taarifa za kufanya mchujo wa makocha 52 waliokua wameomba nafasi hiyo na kubakisha majina machache.
FERWAFA tayari wameshawafanyia usahili makocha kutoka barani Ulaya ambao wamehi kufundisha soka kwenye baadhi ya nchi za Afrika ambao ni Jose Rui Lopes Aguas (Ureno), Raoul Savoy (Uswiz), Peter James Butler (England) na Antoine Hey (Ujerumani).
FERWAFA walivunja mkataba na kocha Jonny McKinstry kutoka Ireland la kaskazini mwezi Agosti mwaka jana.