Meneja wa klabu ya Borussia Dortmund Thomas Tuchel amemkingia kifua mshambuliaji wake kutoka nchini Gabon Pierre-Emerick Aubameyang, kufuatia kitendo cha kukosa mkwaju wa penati katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Benfica.

Katika mchezo huo Borussia Dortmund walikubali kufungwa bao moja kwa sifuri, na kama Aubameyang angepata mkwaju wa Penati huenda matokeo yangekua sare ya bao moja kwa moja.

Thomas Tuchel aliwaambia waandishi wa habari kuwa, suala la mshambuliaji huyo kukosa mkwaju wa Penati ni la kawaida na haoni sababu ya kuanza kuzongwa, wakati tukio hilo lilikua sehemu ya mchezo wa jana.

Utetezi huo wa Tuchel kwa Aubameyang pia umeelekezwa kwa mashabiki wa Borussia Dortmund, ambao walionyesha kukerwa na kitendo cha kukosa kwake Penati ambayo waliiona kama mkombozi wa kujikwamua na matokeo ya kufungwa bao moja kwa sifuri.

Katika hatua nyingine, Tuchel ameahidi kufanya jitihada za kukiandaa vyema kikosi chake kuelekea mchezo wa mkondo wa pili, kwa kuamini bado wana nafasi ya kutinga kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mbingwa barani Ulaya.

Mchezo wa mkondo wa pili kati ya Borussia Dortmund dhidi ya Benfica umepangwa kuunguruma majuma mawili yajayo nchini Ujerumani.

Samson Siasia Aanza Kutajwa Rwanda
Marseille Yavunja Mkataba Na Lassana Diarra