Wizara ya Afya inaendelea na kampeni ya chanjo ya Surua kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano na safari hii Mganga wa Tiba Asili wa kijiji cha Ikulwe kata ya Majimoto Halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele Mkoani Katavi, Mihangwa Lubana ‘Halawa’, ameruhusu watoto wake 12 kupatiwa chanjo ya Surua.

Akizungumza nyumbani kwake mara baada ya kutembelewa na wawakilishi kutoka wizara ya afya na wawakilishi wa Halmashauri, Lubana amesema amehamasika baada ya kupata ujumbe wa elimu ya ugonjwa na chanjo ya Surua, wa Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya.

Amesema, “Nimekuwa nikisikia tu matangazo kwenye magari na ujumbe mkubwa nilioupata ni kwamba si Magonjwa yote yanatibiwa kwa waganga wa Tiba Asili hasa ugonjwa wa Surua, hivyo naishukuru sana Wizara ya Afya kwa kuniletea huduma hii nyumbani kwangu.”

Kwa upande wake mke wa Mganga huyo, Holo Salu amesema hatua inayofanywa na Wizara ya Afya ya kutembea nyumba kwa nyumba kutoa huduma ya chanjo ya Surua itafikia watoto wengi hasa wa sehemu za vijijini .

Kampeni ya uhamasishaji wa chanjo ya Surua kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano Mkoani Katavi, ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu baada ya kuripotiwa taarifa za watoto 13 waliopoteza maisha huko Mpimbwe kutokana na ugonjwa huo.

JWTZ yatangaza nafasi za kujiunga na jeshi
Jukwaa la Maendeleo ya Utamaduni lajipanga kukuza Utamaduni