Kocha Mkuu wa England, Gareth Southgate amekiri kikosi chake hakijacheza kwa kuelewana kwenye safu ya ushambuliaji na kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Ukraine kwenye mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Ulaya mwaka 2024.
Oleksandr Zinchenko alifungia Ukraine bao la kuongoza kwenye mchezo huo uliochezwa Poland kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Lakini beki Kyle Walker aliisawazishia England na hilo kuwa bao lake la kwanza kwenye mechi za kimataifa.
“Hatuwezi kushinda kila mechi kwa mabao manne au saba” alisema Southgate.
“Hicho kilikuwa kipimo kizuri, nje ya nyumbani, kwenye mazingira yaliyoleta hisia kubwa, na mabadiliko machache nilifanya kutoka kwenye kikosi kilichocheza mchezo uliopita.”
Wakati fulani, hasa mnapocheza mchezo wa kushambulia, hatukuwa na maelewano. Tunajua kazi tuliyofanya wiki hi ndio hiyo kila mara tunafanya, haikuwa tofauti.”
Sare hiyo inaifanya England kuhitimisha rekodi yake ya ushindi wa asilimia mia moja kwenye Kundi C baada ya kuwa imeshinda mechi zake zote nne zilizopita.
Bado wako kwenye nafasi nzuri kwani wanaongoza kundi kwa kuwa na pointi 13, sita mbele ya Ukraine inayoshika nafasi ya pili.
England walikumbana na mazingira yaliyowapa hofu huku wapinzani wao Ukraine wakishangiliwa na mashabiki 40,000 waliofurika kwenye uwanja wa Tarczynski Arena.
“Nafikiri nilichovutiwa nacho ni jinsi tulivyotawala mchezo hasa unapokutana na mazingira yenye presha” aliongeza Southgate.
“Nadhani tulicheza kwa utulivu mkubwa mpaka kwenye robo tatu ya mwisho ya wapinzani wetu na nafikiri wakati tunafunga bao tulimiliki mpira kwa asilimia 70 lakini hilo lilikuwa jaribio letu la kwanza lililolenga lango.”