Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetakiwa kuendelea kutenda haki katika kuratibu mchakato wa ajira ili kuiwezesha Serikali kupata watumishi wenye sifa stahiki na maadili mema ambao watatoa huduma kwa umma kwa kuzingatia weledi. .

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa wakati akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo iliyopo Magogoni jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo ambacho kinatakiwa kutenda haki ili Serikali ya Awamu ya Tano ipate watumishi wenye sifa na vigezo watakaoendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ya kuliletea taifa maendeleo katika sekta za miundombinu, afya, viwanda, biashara, kilimo, usafiri wa anga, elimu na  uchumi kwa ujumla wake.

Aidha, amesema kuwa, awali Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilikuwa ikilalamikiwa sana kuwa, mchakato wa kuomba kazi Serikalini ulikuwa ukichukua muda mrefu kiasi cha waombaji kusahau kama waliwasilisha maombi, hivyo ameipongeza Sekretarieti kwa kubuni mfumo wa upokeaji wa maombi ya kazi (Recruitment Portal) na mfumo wa kupanga wasailiwa waliofaulu ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na waombaji wa ajira Serikalini.

Dkt. Mwanjelwa ameitaka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kutobweteka kwa mafanikio waliyoyapata kupitia mfumo wa Ajira Portal na badala yake waongeze kasi ya ubunifu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imedhamiria kwa dhati kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma nchini.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier M. Daudi, amesema kuwa ofisi yake ilianzishwa kwa lengo mahususi la kukabiliana na changamoto za ajira zilizokuwa zikijitokeza hapo awali, hivyo iliundwa ili kuongeza uwazi, kutenda haki na kuhakikisha kuwa ajira zinapatikana kwa kuzingatia sifa.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Mbarak Abdulwakil amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa nasaha zake za kuitaka Sekretarieti kuzingatia weledi katika jukumu zito la kuwezesha ajira za watumishi wa umma na kumhakikishia kuwa, maelekezo yote  aliyoyatoa yatatekelezwa kikamilifu na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 21, 2019
Wakazi wa Itengelo walalamikia kero ya Dampo