Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetakiwa kuwapa wataalamu wa sekta ya maendeleo ya jamii jukumu la kusimamia mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) Iliyoboreshwa katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Wizara hiyo Seleman Jafo wakati akifunga Kongamano la mkutano mkuu wa mwaka wa wataalamu wa sekta ya maendeleo ya jamii lililofanyika jijini Dodoma na kuwataka wataalam hao kutumia taaluma walizonazo kufanikisha zoezi hilo.
Amesema kazi hiyo imekuwa ikifanywa na wataalamu wa sekta ya Afya ambao kitaaluma wana fani ya tiba na madawa lakini linapokuja suala la uhamasishaji wa jamii kushiriki masuala ya maendeleo jukumu hilo huwaangukia wataalamu wa maendeleo ya jamii.
“Wataalamu wa maendeleo ya jamii ni watu ambao wamekuwa hawapewi kipaumbele na kudhalauliwa katika maeneo yao ya kazi lakini umefika wakati wa kuwapatia vitendea kazi na kuwatumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa,” amefafanua Waziri Jafo.
Aidha amesema wataalamu hao wamekuwa hawatumiki ipasavyo katika shughuli mbalimbali zaidi ya zile za dharula au wakati kitaaluma watumishi wengi wa serikali ni wasomi, wenye utaalamu na waliobobea katika kazi.
Kufuatia hatua hiyo Jafo ameagiza mamlaka zilizo chini ya Serikali za mitaa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa wataalamu wa sekta ya maendeleo ya jamii ikiwemo kuwapatia magari ili waweze kufuatilia kazi zao kwa uhakika.
“Na mara baada ya kuboreshwa kwa mazingira ya kazi nawataka wataalamu hawa wa maendeleo ya jamii katika utendaji kazi wao kuhakikisha wanasimamia misimamo katika vikao vya mbalimbali vya maamuzi ili waweze kukubalika na kuaminika,” ameongeza Waziri Jafo.
Awali akiongea mahala hapo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema kongamano la wataalamu wa maendeleo wa jamii limekuwa na mada ambazo kimsingi zitawaletea mabadiliko katika utendaji wao wa kazi ili kujiletea maendeleo kitaifa.
Wataalamu hao wa sekta ya maendeleo ya Jamii wamekutana Jijini Dodoma katika mkutano mkuu wao wa mwaka kwa lengo la kukumbushana majukumu yao sambamba na kupata maarifa mapya kutokana na mada mbalimbali zilizotolewa katika kongamano hilo.