Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (European Investment Bank-EIB) imekubali kuongeza kasi na wigo wa maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Benki hiyo.

Hayo yameelezwa wakati wa mazungumzo baina ya Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na kwenye Umoja wa Ulaya, Jestas A. Nyamanga na Mkuu wa ukanda wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa benki hiyo, Diederick Zambon yaliyofanyika hivi karibuni kwenye Ubalozi wa Tanzania, Brussels.

Katika mazungumzo hayo, wawili hao wamejadili kwa kina juu ya miradi mbalimbali na fursa nyingine zinazoweza kunufaisha Tanzania kupitia mikopo nafuu inayotolewa na Benki hiyo.

Miongoni mwa miradi iliyojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa awamu ya pili ya mradi wa kuboresha msongo mkubwa wa umeme katika vituo vya Iringa na Shinyanga TBIP II.

Wawili hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi kwenye utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga na Kigoma pamoja na ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Sumbawanga. Mradi huu pia unafadhiliwa na Benki ya EIB kwa mkopo nafuu wa Euro milioni 50.

Ujumbe wa Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Bw. Zambon unatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mwezi huu wa Oktoba au mwanzoni mwa Mwezi Novemba mwaka huu kwa ajili ya kuendeleza majadiliano na Serikali pamoja na sekta binafsi kwenye masuala haya muhimu kwa uchumi wa Tanzania.


EIB ni miongoni mwa wadau wakubwa wa maendeleo wa Tanzania na imekuwa ikishirikiana na Serikali na sekta binafsi katika utoaji wa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali nchini.

Video: Warembo wahalifu hatari zaidi, ‘chinjachinja’, omba usikutane nao
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Oktoba 12, 2021