Seneta wa Marekani, Chris Coons aliyezuru nchini Kenya amesema amefanya maongezi na Rais Kenyatta na kumtaka kufanya mabadiliko ya amani ya kimamlaka, licha ya uwepo wa mzozo wa hivi punde juu ya uchaguzi wa kidemokrasia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Coons, amesema, maongezi yake na Rais Kenyatta yalikuwa ni ya matumaini ambayo ana imani yataleta mabadiliko na kudumisha amani iliyokuwepo kuanzia mwanzoo wa kampeni hadi tangazo la Rais mteule William Ruto kutolewa na IEBC.
Amesema, akiwa nchini Kenya alijadiliana na Rais Uhuru Kenyatta njia ambazo anaweza kutekeleza jukumu la kujenga amani, baada ya kuondoka ofisini kipindi kifupi kijacho na kumuacha mrithi wake atakayeendeleza mazuri ya Taifa hilo.
Kenyatta alikuwa kimya na hakuonekana hadharani akiongea tangu uchaguzi wa Agosti 9, kitendo ambacho kiliongeza wasiwasi na kusababisha hali ya sintofahamu baada ya uchaguzi na uwezekano wa pingamizi la mahakama linaloandaliwa na mgombea aliyeshindwa, Raila Odinga.
Coons, akiongoza ujumbe wa bunge katika ziara ya Afrika, alikuwa nchini Kenya kukutana na vyama muhimu vya kisiasa kujadili mambo mbalimbali na kuhimiza hali endelevu ya utulivu uliokuwepo tangu awali.
Ujumbe wa Marekani pia ulitembelea kituo cha matibabu katika mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi, unaofadhiliwa kwa ushirikiano na Marekani ambapo pia Coons, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Seneti kuhusu Mahusiano ya Kigeni, pamoja na ujumbe alioongozana nao tayari wamezuru visiwa vya Cape Verde na Msumbiji na wanatazamiwa kufika nchini Tunisia.