Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022 itahusisha watu watakaolala nchini kuamkia siku yenyewe ya sensa.
Amesema hayo leo Septemba 14, 2021 jijini Dodoma kabla ya kuzindua uelimishaji na mkakati wa uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi, ambapo amesema sensa ni muhimu kwani inakwenda kusaidia utekelezaji wa mipango ya Serikali.
“Taarifa za Sensa zinatumiwa pia na taasisi za Kimataifa, taasisi za kiraia, pia wawekezaji hutumia taarifa hizi kuamua ni aina gani ya biashara kuwekeza na wapi, watafiti wa ndani na nje ya nchi hutumia taarifa za sensa kwa ajili ya tafiti mbalimbali.” amesema Rais Samia Suluhu.
“Kuna hoja nimekuwa nikizisikia kwa nini tutumie pesa zetu nyingi kwa ajili ya Sensa, ni vyema ukawa na taarifa zako kuliko kutumia taarifa za watu wengine, unapotoa taarifa unasema chanzo ni SensaYaTanzania iliyofanyika mwaka flani. Kuliko kusema chanzo ni taasisi flani” amesema Rais Samia
“Huwezi kushughulikia tatizo la ajira kama huna taarifa sahihi kuhusu watu wasio na ajira, huwezi kushughulikia suala la wenye uhitaji maalum bila kufahamu taarifa zao na idadi yao,” amesema Rais Samia.