Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa Watanzania na ina lengo la kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zitakazowezesha kusogeza huduma muhimu kwa jamii.
Dkt. Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema hayo hii leo Agosti 23, 2022 jijini Mbeya baada ya kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi na kuwatoa hofu wananchi kuhusiana na maswali watakayohojiwa na makarani wa Sensa.
Amesema, “Sensa ni muhimu kwa Watanzania maana Serikali inataka kufahamu takwimu sahihi ili kusogez huduma kwa jamii na mimi nimeshahesabiwa, niwatoe hofu tu Watanzania maswali yanayoulizwa ni ya kawaida na yana lengo la kujenga nchi,” amesisitiza Spika wa Bunge.
Miongoni mwa maswali yanayoulizwa na Makarani wa Sensa ni pamoja na umiliki wa simu ambao unalenga kupata taarifa za mhusika na kujiridhisha iwapo kama maofisa wa sensa wamewafikiwa watu waliohesabiwa.