Taarifa zinaeleza kuwa mshauri mkuu ndani ya Klabu ya Young Africans kwenye mchakato wa kuelekea mabadiliko Senzo Mazingiza Mbatha anashikiliwa na Polisi katika kituo cha Oysterbay jijini Dar es salaa kwa tuhuma za kuihujumu klabu ya Simba SC.
Leo mchana taarifa hizo zilitanabaisha kuwa Mazingiza ambaye alikuwa Mtedaji Mkuu wa Klabu ya Simba, alifikishwa kwenye kituoni hapo na kuhojiwa kuhusu ishu ya kudaiwa kuwahujumu mabingwa hao wa Tanzania Bara, ili wapate matokeo mabovu kwenye michezo ya Ligi kuu iliyopita.
Mbatha anadaiwa kufanya hivyo kwa kushirikiana na Hashim Mbaga, aliyekuwa mkurugenzi wa mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba ambaye naye alifutwa kazi siku kadhaa zilizopita.
Simba SC ilipoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons kwa kufungwa bao moja kwa sifuri kisha dhidi ya Ruvu Shooting walioibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri.
Kutokana na hali hiyo uongozi wa Simba SC ulifanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi kwa kumuondoa Mohamed Mwarami aliyekuwa kocha wa makipa pamoja na Patrick Rweyemamu ambaye alikuwa ni Meneja wa Simba.