Aliyekua Afisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Senzo Mbatha Mazingiza, amesema anaiona klabu hiyo ikitinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu kutokana na ubora iliouonesha.
Senzo ambaye kwa sasa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa ‘CEO’ katika Shirikisho la Soka Botswana, anakumbukwa kwa utendaji wake wenye mafanikio ndani ya klabu za Simba SC na Young Africans akiwa hapa nchini.
Senzo amesema kwa kiasi kikubwa ubora ambao wameuonesha Young Africans katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu, wana uwezo mkubwa wa kusonga mbele na kutinga hatua inayofuata ya Nusu Fainali.
“Young Africans mpaka sasa wamecheza vizuri sana, ukiwatazama kwa jinsi ambavyo wameingia Robo Fainali utabaini ni timu ambayo ina nguvu kubwa sana katika michuano hii, ninaamini watafika mbali zaidi ya walipofika sasa.”
“Young Africans wanaweza kutinga Nusu Fainali, uwezo huo wanao, hata wapinzani ambao watakutana na Young Africans katika Robo Fainali wote nikiwaangalia naona kabisa wanayo nafasi ya kufika mbali, natamani kuona Young Africans ikifika hata Fainali ya michuano hii,” amesema kiongozi huyo
Tayari Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeshapanga Droo ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani humo, ambapo Young Africans imeangukia mikononi mwa Mabingwa wa Soka nchini Nigeria Rivers United.
Young Africans itaanzia ugenini nchini Nigeria na baadae itamaliza mchezo wa mkondo wa pili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam mwezi huu.