Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania imeendelea kuweka mikakati na sera endelevu za uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira ikiwemo kuhamasisha zoezi la upandaji miti ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo (Juni Mosi, 2023) Jijini Dodoma, Dkt. Jafo amesema katika kipindi cha mitatu ajenda ya mazingira ni miongoni mwa vipaumbele muhimu vinavyoendelea kupewa msukumo na Serikali ikiwemo uhamasishaji wa kampeni za usafi wa mazingira na upandaji miti.
Amesema, katika siku za hivi karibuni,Tanzania imeshuhudia athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi ambazo ziliathiri sekta mbalimbali za uchumi na uzalishaji mali na kushuhudiwa kuongezeka kwa bei za bidhaa za mazao ya chakula hali iliyotokana na na ongezeko kubwa la ukame katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Sote ni mashahidi kuwa hivi karibuni tumeshuhudia mvua zisizo na wastani mzuri zikinyesha katika baadhi ya maeneo ambazo zilileta athari ikiwemo vifo. Pia tumeshuhudia ukame mkali katika Wilaya za Simanjiro, Longido na Kiteto hali iliyosababisha vifo vingi vya wanyama na kusababisha hali ya umaskini wa kipato kwa wafugaji” amesema Dkt. Jafo.