Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili madawa ya kulevya na uhalifu, Ghada Waly amesema pamoja na kufanya tafiti za kuelewa vema uhusiano kati ya uhalifu wa kupangwa na ugaidi Afrika, ni muhimu pia kuwa na sera na miradi ya kukabili vitendo hivyo vya kiharamu.
Bi. Waly, amesema hayo wakati akihutubia kwa njia ya video mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu amani na usalama barani Afrika, wa kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa maliasili ambao hufadhili makundi yaliyojihami na magaidi.
Amesema, “asilimia 60 ya watu wengi barani Afrika wana umri wa chini ya miaka 25. Vijana ndio mustakabali wa bara hili na pia ndio wako hatarini lakini tunafahamu kuwa vijana wakiwezeshwa, ni waleta mabadiliko, wajengaji wa mustakabali bora, na kuchechemua kwa niaba yao, na kwa niaba ya jamii yao na pia kulinda maliasili.”
Waly ameongeza kuwa, “Tunajengea uwezo vijana kuwa wajenzi wa amani kwenye maeneo ya mipakani ya Gabon, Cameroon na Chad na lengo la mradi huu ni kujenga mtandao wa vijana 1800 wajenzi wa amani, ili wazuie mizozo, ujenzi wa amani kwenye maeneo ya mpakani, na kuwawezesha kuibua mbinu mbadala za kujipatia kipato kwa jamii za mipakani.”
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa UNODC, biashara haramu ya pembe za ndovu pekee huzalisha kipato haramu cha dola milioni 400 kila mwaka huku Afrika ikiwa na idadi ya watu takribani bilioni 1.3, kati yao milioni 500 kwa mwaka jana waliishi kwenye ufukara huku biashara hiyo haramu ikizuia mapato ya maliasili, kuchochea mizozo na ukosefu wa utulivu.